Online

Saturday, November 25, 2017

MAKALA: Namwandikia Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa


Nimejikuta nimekabwa na hamu kubwa ya kukuandikia Mkuu wa Mkoa wa Mtwara japo sina mambo mengi sana yatakayonifanya nikuchoshe kwa kuyasoma lakini nadhani katika hiki nilichoamua kukiandika utapata jambo hata dogo tu la kulifanyia kazi ingawa nitalazimika kuliandika jambo lenyewe kwa namna ya pekee.

Awali, niseme karibu Mtwara – mkoa unaotajwa kuwa mmoja wa wazalishaji wa zao la korosho. Pia ndiyo Mkoa wa nyumbani kwa gesi asilia. Karibu sana!
Kubwa na msukumo wangu wa kukuandikia unatokana na hitaji kubwa sana la wanaMtwara hasa wanamichezo. Jambo hili limezungumzwa sana na watu wa namna mbalimbali; wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi.

Unapozungumzia soka la Tanzania huwezi kuiweka nyuma Mtwara – unaanzaje kwa mfano? Hakuna njia utakayoepa kuitaja Mtwara katika mustakabali wa soka la Tanzania.
Mpira huunganisha watu pamoja wakasahau itikadi zao za vyama, dini, na ukabila. Mpira ni silaha kubwa sana ya kuwaunganisha wakasahau tofauti zao za kibiashara. Wakashikana mikono kushangilia kwa pamoja na wakati mwingine huhuzunika pamoja pale timu yao inapokosa matokeo mazuri.

Nikuhakikishie kwamba watu wa Mtwara wanapenda sana michezo hasa mpira wa miguu na timu pekee ambayo ndiyo kimbilio lao ni Ndanda FC. Hii ndiyo timu pekee inayounganisha Wilaya zote sita za Mkoa wa Mtwara. Ikawakusanya Waislam na Wakristo; wanaCCM, CHADEMA, CUF, NCCR-MAGEUZI na makabila yote yaliyopo Mtwara, wakakaa pamoja na kushangilia ushindi na wakati mwingine wakahuzunika kwa kukosa ushindi.
Itazame vizuri Ndanda FC utabaini kitu. Ndanda ina njaa, Ndanda ina kiu, Ndanda inajikongoja, Ndanda kwa muda mrefu inabaki kwenye Ligi Kuu kwa sababu ya mapenzi ya wachezaji na watu wachache wanaojitolea lakini haifikii mahitaji yao ya msimu. Miongoni mwa timu ambayo ilitakiwa kuwa na mafanikio mazuri zaidi hasa linapokuja suala la udhamini mnono ni pamoja na Ndanda.

Nilikuwa mmoja wa watu waliohudhuria katika Ukumbi wa Boma Mtwara, Novemba 21 siku ambayo ulikutana na Wazee wa Mtwara kujadili changamoto mbalimbali. Yalizungumzwa mengi sana lakini hili la michezo hasa Ndanda FC lilizungumzwa kwa hisia kali sana na wachangiaji wake. Miongoni mwa walioumizwa na mwenendo wa timu hiyo ni Mama Mangasara ambaye aligusia mpira kama sehemu ya ajira ambayo wengi wenye vipaji wamekuwa wakinufaika.

Kama mpira ni kipaji kwa Tanzania hapa ni Ligi Kuu pekee ambayo matunda ya kipaji cha mtu huonekana. Hivyo chini ya hapo hakuna kitu. Nakumbuka maneno ya mama Mangasara alipokuwa akizungumzia mpira, alisema: “Maendeleo ya Mikoa ya Kusini ni mpira. Na mpira ni ajira na ni vijana tunawaambia wajishirkishe huko.”

Hapa utaona ni namna gani mpira unavyoweza kuleta manufaa mbali ya kuwa burudani kwa watazamaji – mpira ni ajira. Nikupe mfano mdogo tu hapa. Timu ya mpira inasajili wachezaji 30. Maana yake tayari watu 30 kutoka familia tofauti wameajiriwa. Mbali na wachezaji wapo pia makocha, meneja wa timu, Afisa Habari. Hapa tayari umeshatengeneza ajira ya watu zaidi ya 35 na kushuka kwake maana yake ajira hizo zimepotea. Lakini kwa nini ishuke daraja wakati uwezo wa kuifanya itambe ungalipo?

Timu kushuka daraja maana yake ni anguko kubwa la Mkoa wote. Halitokuwa anguko la wanasiasa pekee wala wafanyabiashara pekee bali ni Mkoa wote. Na hakuna shughuli kubwa sana kama kuipandisha timu Ligi Kuu. Nakumbuka mama yule alisema; “Mpira upo kama siasa, ukianguka mwaka huu kutafuta kupanda daraja shughuli yake pevu.” Ni kweli kabisa.
Mtwara ilisubiri zaidi ya miaka 10 kuipata timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania baada ya iliyokuwa timu pekee Bandari kushuka daraja mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Ni wewe, viongozi wengine wa mkoa, wadau wa michezo, viongozi wa Ndanda na wanaMtwara wote wanatakiwa kuhakikisha hii timu inakuwa katika hali nzuri.

Nilifurahi kukuona Nangwanda Sijaona kuhamasisha wanaMtwara lakini hii haitoshi, kubwa zaidi iangalie timu isiwe ombaomba, isiwe yatima. Uifanye timu hii iwe kimbilio la vijana wengi kwa ajili ya kujipatia ajira kutokana na vipaji vyao. Ifanye timu hii iwe suluhisho la mustakabali wa watu wa Mtwara. Ifanye iwaunganishe watu wote bila kujali itikadi za kisiasa wala kidini.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa (katikati, waliokaa) akiwa na baadhi ya viongozi wa dini alipokutana na Wazee wa Mtwara November 21, 2017 katika ukumbi wa Boma, Mtwara

Friday, November 17, 2017

MAHAKAMANI: Jalada kesi ya Aveva na Kaburu larudishwa tena TAKUKURU


Jalada la kesi ya utakatishaji fedha wa USD 300,000, inayowakabili Rais wa Simba SC, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange Kaburu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lipo mikononi mwa TAKUKURU kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.

Awali, TAKUKURU ililipeleka jalada hilo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kulikagua kuhusu suala la upelelezi.

Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Leornad Swai amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa kesi bado haujakamilika.

>>>"Jalada limerudi kwetu juzi na ametoa maelekezo tena kuhusu upelelezi."

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mwambapa ameahirisha kesi hiyo hadi November 30, 2017.

Aveva na makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha USD 300,000.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa  USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.

Katika shtaka la pili alidai kuwa Machi 15, 2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016 wakati akijua ni kosa.

Katika la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29, 2016 Dar es Salaam  kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15, 2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa  Machi 15, 2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva  kujipatia USD 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

Monday, May 22, 2017

Marafiki wa NDANDA F.C 3-0 Wanafiki wa NDANDA F.C


HAKUNA kitu kizuri kama kushinda vita – kumshinda adui yako ni moja kati ya vitu vinavyofurahisha nafsi katika hali ya upeo wa juu sana. Unapomshinda adui yako unamaanisha ushujaa wako katika kila hali. Unakuwa umemshinda kwenye mbinu za kupigana. Kama haitoshi, unakuwa umemshinda kwenye namna ya uwezo wa kupambana.
Kwa hivi pia unakuwa umemdhalilisha – na hakuna kitu ambacho wengi hawakipendi kama kudhalilishwa. Watu walioshindwa vita hushindwa kila kitu; hujiona wako chini na hawawezi hata kuinua sauti mbele yako. Hujiona wamekuwa dhaifu mbele yako kwa sababu kwanza umempiga lakini pia umejua udhaifu wake.

Kwa namna hii ndivyo ilivyokuwa kwa marafiki wa Ndanda FC ambao wakati huu wanafurahia ushindi wao wa 3-0 dhidi ya wanafiki wa Ndanda FC. Hakuna kitu kinachowafurahisha kama kuwaziba midomo wanafiki – hili ndilo bao la kwanza. Wapo waliokuwa wanaomba kila siku Ndanda FC ishuke daraja kwa sababu wanazozijua wao wenyewe. Ndanda FC kusalia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ni ushindi mkubwa kwa marafiki wa Ndanda.
Bao la pili kwa marafiki wa Ndanda dhidi ya wanafiki wa Ndanda linakuja pale ambapo wengi walidhani kutokana na ukata mkubwa uliowasumbua kwa muda mrefu timu hiyo ingeshindwa kufurukuta katika kumalizia duru la pili Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ni katika kipindi ambacho kila mtu alikuwa anaisubiri May 20 kuthibitisha kuwa Ndanda FC imerudi rasmi Ligi Daraja la Kwanza.

Bao la tatu wanafiki wa Ndanda wamefungwa pale walipojisahau wakidhani kuwa Ndanda FC ilikuwa timu ya mtu mmoja. Walisahau kuwa kundi lao dogo la kuipinga timu hiyo lilitosha kuifanya Mtwara kuamini hawakuwa na timu kutokana na matokeo ya uwanjani. Kwa hivi ilikuwa kila siku ikicheza wao walisema “Ndanda hakuna timu. Itashuka tu Daraja.” Walisahau kuwa kila wao walipoomba dua kwa Mungu aishushie maafa timu hiyo, wapo wengi wengine walioiombea mema timu hiyo. Kwa nini wasifungwe?

Wakati ule ilikuwa ngumu sana kwa watu kunielewa nilipoandika kuwa Mtwara tunaihitaji zaidi Ndanda F.C. Wapo ambao walidiriki kusema kwa wazi kabisa kuwa hakuna aliyeihitaji timu hiyo. Hawa ndiyo wanafiki wenyewe – wanafiki ambao wameshafungwa 3-0 na marafiki wa Ndanda.

Nadhani itoshe kuwa kilichotokea kwa Ndanda FC msimu uliopita kuwa funzo kubwa sana kwa Mkoa wa Mtwara – mkoa ambao una historia kubwa sana katika soka la Tanzania. Uvumilivu uliofanywa na Viongozi, wachezaji na mashabiki wa Ndanda ni wa hali ya juu ambao unapaswa kupongezwa kwa nguvu zote.

Bado naamini na nasisitiza kuwa Mtwara tungali tunaihitaji Ndanda FC kuliko Ndanda FC inavyoihitaji Mtwara. Kwa namna yoyote iwayo huu ndiyo wakati pekee wa kuonesha kuwa umoja upo miongoni mwa wanamichezo wa Mtwara – unafiki hauna tija.


Hawawezi kujionesha sasa kwamba wao ndiyo walikuwa mstari wa mbele kuiombea mabaya Ndanda FC lakini wanajulikana. Wakati huu watafurahi na Marafiki halisi wa Ndanda kwa sababu lengo lao limeshindikana. Wanaumia na wataumia zaidi kuiona Ndanda ikiendelea kufanya vizuri miaka mingine ijayo.

Tuesday, February 28, 2017

EPL: Leicester City 3-1 Liverpool: Jamie Vardy afufuka kwa Reds

Leicester ilicheza vizuri kwenye mchezo wao wa kwanza tangu kufutwa kazi kwa meneja Claudio Ranieri, wakijondoa kwenye eneo la hatari kwenye Premier League baada ya mabao mawili ya Jamie Vardy na bao la Danny Drinkwater kuisaidia timu hiyo kuirarua Liverpool mabao 3-1.
Ilikuwa katika kiwango kizuri chini ya mlezi Craig Shakespeare, ambaye alichukua majukumu ya meneja aliyewaongoza kutwaa taji la Premier League msimu uliopita.
Bao la kufutia machozi kwa Liverpool lilifungwa na Philippe Coutinho.
Mabao hayo yanakuwa ya kwanza kufungwa na Foxes kwenye ligi mwaka 2017 na kumaliza mbio za mechi tano bila ushindi.
Liverpool - ambayo wangaliweza kupaa hadi nafasi ya tatu kama wangalishinda - sasa wamepoteza mechi tano kati ya saba kwenye mashindano yote.

Ndidi afanya ya Kante - dondoo muhimu kuzifahamu

  • Leicester imeshinda mechi zote sita za Premier League ambazo walitangulia kufunga msimu huu, rekodi ya 100% kwenye ligi hiyo.
  • Vichapo vinne kati ya vitano kwa Liverpool kwenye Premier League msimu huu wamevipata kutoka kwa timu ambazo zilikuwa katika hatari ya kushuka daraja (pia Burnley, Swansea na Hull City).
  • Bao la Vardy lilikuwa la kwanza kwa Leicester kwenye ligi tangu 31 Disemba, likimaliza dakika 637 bila bao.
  • Bao la Coutinho lilikuwa bao lake la kwanza kwenye mechi 12 kwa Liverpool - mara ya mwisho kufunga ilikuwa dhidi ya Watford Novemba.
  • Wilfred Ndidi alifanya tackle 11 Jumatatu. Ni kiungo wa zamani wa Leicester N'Golo Kante pekee - sasa anakipiga Chelsea - amefanya tackle nyingi zaidi kwenye mchezo mmoja wa Premier League msimu huu (14 dhidi ya Liverpool Januari).
  • Ni mwaka 2012 pekee, ambapo walivuna pointi tano, Liverpool walivuna pointi chache zaidi kwenye mechi tano za mwanzo wa kalenda ya mwaka kwenye Premier League dhidi ya saba walivuna hadi sasa mwaka 2017 (sawa na mwaka 1993).

Kifuatacho?

Leicester itawaalika Hull City Jumamosi katika dimba la King Power, ukifuatia mchezo wa marudiano wa Champions League hatua ya 16 dhidi ya Sevilla 14 Machi.
Liverpool watawaalika Arsenal Jumamosi na watakuwa nyumbani tena Jumapili inayofuata watakapowaalika Burnley.

Monday, February 27, 2017

Serie A: Inter Milan 1-3 AS Roma: Radja Nainggolan apiga mbili Roma ikiifuata Juventus

Radja Nainggolan alifunga mara mbili AS Roma ikiichapa Inter Milan mabao 3-1 na kuhuisha matumaini ya kutwaa taji la Serie A.
Mshambuliaji wa Ubelgiji alifunga bao la kuongoza dakika za mapema kabla ya kukimbia na mpira kuanzia katika nusu yao na kufunga bao la pili kwa shuti la umbali wa yadi 25.
Mauro Icardi aliipa matumaini Inter inayokamata nafasi ya sita alipofunga bao akiunganisha krosi ya Ivan Perisic.
Lakini mkwaju wa penalti uliopigwa na Diego Perotti baada ya Gary Medel kumuangusha kwenye box Edin Dzeko ukahitimisha karamu ya mabao kwa Roma.
Vijana wa Luciano Spalletti, ambao wameshinda mara nane kwenye mechi tisa zilizopita kwenye Serie A, wako ya vinara Juventus kwa pointi saba zikisalia mechi 12.
Kwingineko kwenye Serie A, Palermo walitoka sare ya bao 1-1 na Sampdoria huku Chievo wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Pescara wakati Crotone ikichapwa mabao 2-1 na Cagliari na Genoa ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Bologna. 
Lazio ikaibamiza Udinese bao 1-0 na Sassuolo ikalala kwa bao 1-0 kutoka kwa AC Milan.
 
Copyright © 2011. The Chief - All Rights Reserved.